Description
Huyu ni Imam Husain bin Ali bin Abu Talib – Madhulumu wa Karbala – mjukuu wa Mtukufu Mtume Muhammad (saww) kwa binti yake Fatima.
Masaibu ya Karbala ni maarufu sana. Kila mwaka unapofika mwezi wa Muharram, Waislamu duniani kote hufanya majlisi (mikusanyiko) kwa ajili ya kuomboleza masaibu yaliyompata Imam Husain (as) – mtoto wa Imam Ali (as) na Fatima (as) ambaye ni mjukuu halisi wa Mtukufu Mtume (saww).
Kwa hakika masaibu haya yanazidi kuwa maarufu kadiri miaka inavyozidi kwenda. Waislamu wanazidi kuathiriwa mno na masaibu haya, na kuwa na hamu ya kutaka kujua zaidi masaibu haya yaliyompata mjukuu huyu wa Mtukufu Mtume (saww) yametokana na nini na
yamesababishwa na nini hasa.
Kama ilivyo vitabu vyingi vinavyohusu masuala ya dini vimeandikwa kwa lugha za kigeni, vivyo hivyo maelezo ya masaibu haya mengi yamo kwenye lugha za kigeni, na hivyo Waislamu wengi wazungumzaji wa Kiswahili wamekuwa hawazipati habari hizi moja kwa moja kupitia kwenye vitabu, ila kwa kuhudhuria majlisi. Hivyo ili kuzima kiu ya wasomaji wetu, haya hapa ni maelezo ya tukio hilo (la kusikitisha) kwa lugha ya Kiswahili.





